Na. Afisa habari
Wananchi katani msimbati halmashauri ya wilaya ya mtwara siku ya ijumaa 03 Julai, 2020 wamezuiwa jaribio lao la kuanzisha mgogoro wa kutaka kudai fidia serikalini kutokana na kutwaliwa eneo ilipojengwa shule ya sekondari msimbati.
Zuio hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa wa Mtwara Ndg. Gelasius G. Byakanwa alipokuwa anatoa majibu ya hoja mbalimbali zilizotolewa na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara kushughulikia kero katani msimbati ambapo walitaka kujua serikali italipa lini fidia ya mazao yaliyokuwa katika eneo la shule kwakuwa umepita muda mrefu.
Akitolea maelezo hoja hiyo, mkuu wa mkoa alieleza kuwa, utaratibu unaotumika kutwaa maeneo kwaajili ya ujenzi wa sekondari za kata unafahamika, inatolewa na serikali ya kijiji kwa ridhaa ya wananchi kisha ujenzi unaendelea na hatua zote zinafuata taratibu za kisheria.
Aliongeza kuwa, wanufaika wakubwa wa huduma ya elimu ni watoto wanaotokana na jamii ambayo iliamua kutoa eneo husika kama ilivyojidhihirisha kwa baadhi ya vijana waliotoa michango yao kwenye mkutano huo, wameonesha kutoa michango mizuri sana.
Aliendelea kusema kuwa haoni asili ya mgogoro hapo isipokuwa kwa wale watakaoamua kujitoa ufahamu nje ya utaratibu uliotumika, ndiyo maana kuna mwananchi mwenzao ametoa maelezo mazuri sana yanayofanana na utaratibu wa kisheria uliotumika kutwaa eneo hilo na amethibitisha kuwa ridhaa ilitoka kwao wenyewe hayo mazao yamepandwa baada ya shule kuwepo.
Historia inaeleza kuwa eneo hilo lilitolewa na kijiji mwaka 1994 ili kuruhusu ujenzi wa shule ya sekondari, mara baada ya taratibu zote kufuatwa ujenzi ulifanyika na mwaka 2004 shule ikaanza kuchukua wanafunzi ambapo zaidi ya miongo miwili na nusu hakujawahi kutokea mgogoro, ila kwa sasa wameibuka watu wasiotaka kukubaliana na uhalisia.
Kutokana na maelezo hayo ya kutosha, iliagizwa kuwa eneo lote la shule liheshimiwe, litunzwe hakuna ruhusa kwa mwananchi yeyote kufanya shughuli zake, pia wataalamu wa ardhi wametakiwa kubainisha mipaka ya eneo husika ili kuondoa uwezekano wa wavamizi ambapo zoezi hilo limetakiwa kufanywa kwa maeneo yote ya taasisi za serikali.
Mtwara.
Anuani ya posta: 528.
Simu ya Mezani: 023-2333928
Simu: 023-2333928
Barua pepe: Mtwaradc@mtwara.go.tz
Copyright ©2020 MTWARA DC . All rights reserved.