Na Afisa habari.
Kata za naumbu na msangamkuu halmashauri ya wilaya ya mtwara jana 30 Juni, 2020 zimepata mashine mbili za boti za uvuvi na nguvu ya kuendelea na ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya na elimu mara baada ya kutembelewa na mkuu wa wilaya ya mtwara Ndg. Dunstan Kyobya.
Ziara hiyo imeleta neema katika kijiji cha mgao mara baada ya mkuu wa wilaya kukabidhi mashine ya boti ya uvuvi aina ya Yamaha “Horse Power 40” yenye thamani ya milioni 7.5 kwa kikundi cha vijana cha JIWEZESHE kinachofanya shughuli zake katika eneo hilo, mashine hiyo imetolewa kama ruzuku na wizara ya uvuvi ikiwa ni ahadi waliyopewa na kufuatiliwa na ofisi ya mbunge, wanakikundi wamefurahishwa na ruzuku hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano na serikali.
“Kwakweli sisi tunashukuru sana, tunaishukuru serikali kwa kutupatia mashine hii na fedha taslimu laki tano kutoka kwa mbunge, pia halmashauri ilitupatia mkopo wa vijana wa Tzs. 13,000,000/= kutokana na hayo tukaacha kabisa uvuvi haramu, sasa hivi tunashirikiana bega kwa bega na serikali” alisema ndg. Ali Juma Salumu Katibu wa kikundi.
Aidha, viongozi hao wameunga mkono ujenzi wa jengo la wazazi katika zahanati ya Mgao ambapo kijiji kina jumla ya Tzs. 10,000,000/= huku mbunge akiwaongezea milioni moja, ujenzi huo unatarajiwa kuanza wiki hii kutokana na uhitaji wa jengo hilo.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi mtendaji ndg. Maisha S. Mtipa amesema kuwa, anapongeza juhudi za wananchi pia halmashauri itasaidia kuongeza nguvu zake katika hatua za umaliziaji kwakuwa imetenga kiasi cha fedha kuunga mkono juhudi za wananchi katika miradi kama hiyo.
“Hatuwezi kuacha juhudi za wananchi zipotee bure, kwakuwa mwaka wa fedha 2020/2021 kuna zaidi ya milioni 200 zimetengwa kwaajili ya kusaidia miradi ya nguvu za wananchi kwahiyo tutawaunga mkono ila kwa sasa waanze” aliongea Maisha Mtipa.
Wakati huo huo, mashine ya pili imetolewa kwa kikundi cha MWENDOKASI kinachofanya shughuli za uvuvi katika pwani ya msangamkuu, mwenyekiti wa kikundi hicho ndg. Mzee Musa Malango ameeleza kwamba mapokezi ya mashine hiyo imetegua kitendawili cha muda mrefu kilichokuwa kinawasumbua miongoni mwa vijana kwakuwa wengi wao walihisi haitatekelezwa.
Katika hali isiyo tarajiwa wakati mkutano unaendelea aliibuka mwananchi mmoja aliyemuomba mkuu wa wilaya asimamie harambee ya ujenzi wa shule ya sekondari, harambee hiyo ya dakika 20 ilifanikiwa kupatikana kwa jumla ya Tzs. 1,810,000/=, tofali 2000 na mifuko 50 ya saruji kutoka kwa Mkuu wa wilaya kisha michango ikakabidhiwa kwa mwenyekiti wa kijiji.
Mtwara.
Anuani ya posta: 528.
Simu ya Mezani: 023-2333928
Simu: 023-2333928
Barua pepe: Mtwaradc@mtwara.go.tz
Copyright ©2020 MTWARA DC . All rights reserved.