Na. Afisa Habari
Mapema Jumamosi ya leo, Mkuu wa wilaya ya Mtwara ndg. Dunstan Kyobya ametoa siku 14 kwa mkurugenzi mtendaji wa halamshauri ya wilaya ya mtwara kuhakikisha anamalizia ujenzi wa maboma ya madarasa 15 ya shule mbalimbali za sekondari ili kuondoa hadha ya watoto kukosa sehemu ya kusomea.
Ameongea hayo leo katika ukumbi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania tawi la Mtwara (TIA) uliopo mjimwema wakati akitoa mada elekezi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma katika kikao kazi kilichoshirikisha viongozi na watumishi wa halmashauri tatu zilizopo katika wilaya anayoiongoza ambapo ametoa wito wa umaliziaji wa ujenzi huo.
“Nataka hadi kufikia Julai 15 mwaka huu maboma yote ya madarasa 15 yawe yamekamilika na kuanza kutumika ili wanafunzi wote wawepo shuleni kama agizo lilivyoelekeza, kusiwe na sababu zitakazokwamisha masomo” alisema DC Kyobya.
Katika kufanikisha hilo, afisa elimu sekondari ndg. Fadhili Mvungi ameeleza kuwa, kwa sasa mafundi wapo katika ujenzi uliopo katika hatua mbalimbali za umaliziaji maboma na kuezeka ambapo Saruji na tofali zimeshapelekwa shule husika huku Lori mbili za mbao zimeshawasili kwaajili ya kenchi na madawati, bati zimeshafika kutoka kiwandani na fedha zaidi ya milioni 50 zilishatolewa.
Akiongezea maelezo ya utekelezaji wa agizo hilo, kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara ndg Maisha Mtipa amesema kuwa, madarasa hayo yanajengwa katika Shule za Sekondari Ziwani madarasa 4, Mayanga 3, Mahurunga 3, Nanguruwe 2, Ndumbwe 1, Dihimba 1 na Madimba 1 ambapo utengenezaji wa viti na meza kwaajili ya wanafunzi unaenda sambamba na umaliziaji wa madarasa hayo.
Shule za msingi na sekondari zinatarajiwa kufunguliwa Jumatatu ya tarehe 29 Juni mwaka huu mara baada ya kufungwa kwa takribani miezi mitatu na nusu kutokana na mlipuko virusi vya virusi vya CORONA vinavyosababisha ugonjwa wa COVI-19, maandalizi ya mazingira na vifaa vya kujihadhari na ugonjwa huo vimeshanunuliwa na elimu inaendelea kutolewa kwa walimu, wanajamii na wanafunzi.
Mtwara.
Anuani ya posta: 528.
Simu ya Mezani: 023-2333928
Simu: 023-2333928
Barua pepe: Mtwaradc@mtwara.go.tz
Copyright ©2020 MTWARA DC . All rights reserved.